MADA YA SITA: ANDISHI WA INSHA NA MATANGAZO

  MADA YA SITA: ANDISHI WA INSHA NA MATANGAZO

Uandishi wa Insha za Kisanaa
Misingi ya Kuandika Insha
Insha za kisanaa ni insha zinazoelezea mambo ya kawaida katika jamii lakini kwa kutumia lugha ya kisanaa. Lugha ya kisanaa ni pamoja na matumizi ya tamathali za semi, misemo nahau, methali na taswira.
Muundo wa Insha
Kwa kawaida insha inakuwa na sehemu kuu nne: kichwa cha insha, utangulizi, kiini na hitimisho.
  1. Kichwa cha insha; Kichwa cha insha hudokeza kile utachokijadili katika insha yako, hubainisha wazo kuu la mada inayohusika. Kwa kawaida kichwa cha insha huandikwa kwa sentensi fupi. Mfano; maisha ya kijijini, mimba za utotoni.
  2. Utangulizi; Mambo yaliyopo katika utangulizi ni pamoja na kutoa fasili ya maneno muhimu na kuelezea kwa muhtasari mambo ambayo utakwenda kuyajadili katika insha yako. Utangulizi unakuwa katika aya moja fupi.
  3. Kiini cha insha; Katika kiini ndipo kuna maelezo ya kina juu ya kile unachokijadili katika insha yako, maelezo haya yanakuwa katika aya kadhaa kulingana na idadi ya hoja ulizonazo katika mjadala wako.
  4. Hitimisho; Hapa ndipo kuna muhtasari wa kile kilichojadiliwa katika kiini cha insha au inaweza kuwa ni msimamo juu ya kile kilichojadiliwa katika insha.
Insha za Kisanaa
Insha ya kisanaa ni ile inayotumia lugha ya kisanaa yaani yenye tamathali za semi kama vile sitiari, tashbiha, taniaba na mubalagha. Aidha insha ya kisanaa hutumia mbinu nyingine za kisanaa kama tashititi, takriri, na tanakali sauti. Vilevile insha za kisanaa huwa na lugha zenye mvuto na misemo kama nahau, methali na tamathali za semi.

Uandishi wa Matangazo
Tangazo ni taarifa za wazi zinazotoa ujumbe fulani kwa walengwa wanaohusika na ujumbe huo. Ujumbe unaweza kuwa na lengo la kushawishi, kuarifu, kuelekeza, na kadhalika.

Vipengele vya Kuzingatiwa katika Uandishi wa Mtangazo
Malengo ya matangazo
  • Kutoa taarifa;Lengo mojawapo la matangazo ni kutoa taarifa, mfano wa matangazo yanayotoa taarifa ni mialiko, tangazo la kifo, alama za barabarani, matangazo ya kazi.
  • Kuonya; Matangazo pia yana lengo la kuonya, kwa mfano matangazo kama vile ya kutovuta sigara, UKIMWI na kadhalika.
  • Kushawishi; Matangazo pia yana lengo la kushawishi, matangazo yenye lengo hili mara nyingi ni matangazo ya biashara ambayo kwa kweli lengo lake ni kushawishi wateja ili wanunue bidhaa zao, mtangazo ya mialiko hasahasa ya tukio fulani, labda msanii anazindua albamu fulani na kadhalika.
Jinsi ya kuandika matangazo
Ili tangazo liweze kufanikisha kufikia lengo lililokusudiwa kuna mambo kadhaa ya kufanya; mambo hayo ni kama yafuatayo:
  • Kichwa cha habari; Mara nyingi matangazo yanakuwa na kichwa cha habari, hii inasaidia kujua kwa haraka kuwa tangazo linahusika na kitu gani.
  • Kuonesha aina ya bidhaa/huduma; Hiki ndicho kiini cha tangazo, hapa tangazo linaonesha ujumbe uliokusudiwa kufikishwa kwa wahusika, sasa ujumbe huu waweza kuwa ni bidhaa inayotangazwa au huduma inayotolewa au kazi inayotangazwa au mwaliko unahusu nini.
  • Anwani; Hapa tangazo linaonesha mahali ambapo watoa tangazo walipo, yaani ofisi zao zilipo ambapo wahusika wa tangazo wanaweza kwenda na kuwakuta. Kama ni tangazo la mwaliko basi ni lazima lionesha shughuli yenyewe itafanyika wapi.
  • Njia za mawasiliano; Kama ni tangazo la biashara au la kazi au la mwaliko ni muhimu kutoa mawasiliano. Mawasiliano hayo yanaweza kuwa ni namba ya simu, fax, wavuti (kwa taarifa zaidi), barua pepe.
Mbinu za uandishi wa matangazo
Ili tangazo liweze kuvuta umakini wa watu ni lazima liwe na mwonekanao fulani. Zifuatazo ni mbinu za uandishi wa matangazo.
  • Matumizi ya picha; Matangazo mengi ya biashara huwa yanaambatana na picha, picha hizi hujaribu kumshawishi mteja aamini kuwa ile bidhaa ni bora na hivyo ni muhimu kuwa nayo au kuinunua.
  • Maneno machache; Matangazo hutumia maneno machache kwa lengo la kutomchosha mlengwa lakini wakati huohuo maneno hayo yana nguvu ya kumshawishi mlengwa.
  • Lugha ya kisanii; Maneno ya kisanii katika matangazo huwa ni mepesi kukumbukwa na huwa yanaeleweka kirahisi. Kwa mfano, matumizi ya vivumishi, litakuwa ni bonge la shoo, njoo ujinunulie pamba za ukweli, n.k. Matumizi ya mubalagha, kwa mfano; mtandao unaoongoza Tanzania, mganga bingwa afrika mashariki na kati n.k
  • Matumizi ya watu maarufu; Matangazo mengi hususani ya biashara hupenda kutumia watu maarufu ili kuwashawishi walengwa. Kwa mfano kama ni tangazo juu ya bidhaa fulani, huweza kumwonesha pengine msanii maarufu, miss Tanzania, au mchezajia mpira maarufu. Sasa mlengwa anapoona kwamba hata mtu maarufu anatumia hiyo bidhaa, anashawishika na yeye kuitumia






                            MADA YA SABA: KUSOMA KWA UFAHAMU
Kusoma Kimya
Ufahamu wa kusoma ni ule mtu anaoupata kwa njia ya kusoma makala, kifungu cha habari, kitabu au gazeti.

Maswali ya Ufahamu kutokana na Habari uliyosoma
Katika ufahamu wa kusoma, msomaji anatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo:
  • Kubaini mawazo makuu; msomaji anaposoma habari fulani au kitabu inatkiwa ajiluze, Je, kinachoongelewa hapa nini? Ni jambo gani hasa analolizungumzia mwandishi? Msomaji akiwa na maswali haya akilini mwake basi itakuwa rahisi kwake kuielewa habari hiyo.
  • Kuzingatia alama za uakifishi; msomaji ni lazima azingatie alama za uakifishi, kwa kufanya hivyo itamsaidia kuelewa ujumbe wa habari hiyo na endapo hatazingatia alama za uakifishaji anaweza kupotosha maana ya mwandishi.
  • Kubaini maana ya maneno na misemo mbalimbali; habari nyingine huwa zina maneno ya kisanaa hivyo ni muhimu msomaji kubaini maana ya maneno hayo katika muktadha wa habari hiyo, hii itamsaidia kuelewa vyema maana ya mwandishi.
  • Vilevile msomaji anatakiwa kumakinikia kile anachokisoma, kila kipengele anachokisoma inampasa akielewe vizuri.
Kwa kuzingatia haya yote msomaji atakuwa na uelewa mzuri juu ya habari aliyoisoma na pia anaweza kufupisha habari hiyo aliyoisoma

Kufupisha habari
Kufupisha habari ni kuandika upya habari uliyoisoma kwa maneno machache lakini bila kupotosha ujumbe wa habari ya kwanza.
Ufupisho wa habari huwa na sifa hizi:
  • Huwa ni mfupi kuliko habari ya mwanzo
  • Huwa na ujumbe uleule uliokuwa katika habari ya mwanzo
  • Hujumuisha mawazo makuu yaliyodondolewa kutoka kwenye habari ya mwanzo
  • Mawazo haya sharti yapangwe katika mtririko wenye mantiki
Hatua za kufuata katika kuandika ufupisho
Ili kuweza kufanikiwa kufupisha habari kwa ufanisi hatua zifuatzo sharti zifuatwe:
  • Kuisoma au kuisilikiza habari kwa makini ili kuielewa vizuri
  • Kutambua na kubaini mawazo makuu yanayojitokeza katika kila aya
  • Kuyaunganisha mawazo makuu na kuandika au kuelezea ufupisho wa habari hiyo kwa maneno yako mwenyewe bila kupostosha maana ya habari ya kwanza.
  • Kuhesabu idadi ya maneno ya ufupisho ili kuyapunguza ikiwa yanazidi idadi iliyotakiwa.
  • Kama muda unaruhusu pitia tena habari ya mwanzo na pitia tena ufupisho ili kujiridhisha kuwa hujaacha taarifa yoyote ya muhimu.
Kufupisha Habari Uliyoisoma
Mtu mmoja na mkewe kutoka jamii ya Daliti inayobaguliwa tangu jadi nchini India wameuawa, mmoja akiwa amekatwa kichwa na mwengine kunyongwa kwa kushindwa kulipa deni la Rupee kumi na tano ambalo ni karibu senti ishirini na mbili tu.
Polisi kaskazini mwa taifa hilo wamethibitisha kisa hicho ambapo yasemekana mfanyi biashara anayetokea jamii ya hadhi ya juu,aliwaua wanandoa hao kwa kushindwa kulipa deni la biskuti walizokuwa wamewachukulia watoto wao.
Mfanyi biashara huyo amekamatwa.Ubaguzi kwa misingi ya kijamii umeenea sana nchini India, huku watu wa jamii ya Daliti waliokuwa wamebadikwa jina la 'the untouchables' wakiwekwa kwenye daraja la chini kabisa kwenye sera hiyo ya kibaguzi nchini India iitwayo 'caste' ambapo wananyimwa fursa nyingi za kimaendeleo na hivyo kubaki katika lindi la umaskini.
Hata hivyo Visa vya ukatili wa kibaguzi dhidi ya jamii ya Dalit katika jimbo la Gujarat vimeongezeka mnamo siku za hivi karibuni na vimesababisha wimbi la maandamano kutoka watu wa jamii hiyo.

Zoezi
Kwa maneno yasiyozidi 30 fupisha habari uliyoisoma hapo juu.

Comments

Popular posts from this blog

MADA YA TANO: UTUNGAJI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI

Dhana ya Tungo